Klabu ya Azam FC imeendelea kuimarisha kikosi chake baada ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji raia wa Uganda, Hassan Mubiru, akitokea SC Villa kwa mkataba wa miaka miwili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na vyanzo vya karibu na klabu hiyo ya Chamazi, Azam FC imefanikiwa kumuwahi mshambuliaji huyo baada ya kumalizana naye rasmi na kumfanya kuwa sehemu ya kikosi kuelekea msimu ujao wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Ujio wa Mubiru unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Azam FC wa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji, ambayo imekuwa ikihitaji ubunifu na mabao zaidi katika mechi za ushindani mkubwa.
Mshambuliaji huyo anatajwa kuwa na uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja katika eneo la mbele, akitumiwa kama namba 9 au kushuka nyuma kusaidia ujenzi wa mashambulizi.
Kabla ya Azam FC kufanikisha dili hilo, ripoti mbalimbali zilionyesha kuwa klabu kadhaa za Afrika Mashariki zilikuwa zikimwania mchezaji huyo, ikiwemo baadhi ya timu kutoka Rwanda. Hata hivyo, Azam FC imefanikiwa kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho cha usajili.



