Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga SC, Ali Kamwe, amethibitisha rasmi kuwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga dhidi ya Azam FC uliopangwa kupigwa Juni 24 sasa utachezwa katika uwanja wa New Amaan Complex uliopo visiwani Zanzibar.
Yanga SC watakuwa wenyeji wa mchezo huo muhimu ambao una uzito mkubwa katika harakati zao za kutetea ubingwa wa ligi msimu huu.
Ali Kamwe amesema kuwa Yanga tayari imekwishawaarifu rasmi Bodi ya Ligi kuhusu uamuzi wa kubadilisha uwanja na kuhamishia mchezo huo Zanzibar. Uamuzi huo unaonekana kuwa sehemu ya mipango ya kiufundi Yanga ikihitaji kushinda.
Kamwe pia alieleza kuwa baada ya mchezo wa nusu fainali wa Kombe la CRDB Bank Cup dhidi ya Azam FC utakaopigwa Juni 21 katika uwanja wa CCM Kirumba, kikosi cha Yanga kitaelekea visiwani Zanzibar moja kwa moja kujiandaa kwa mtanange hu.
Mchezo huo wa ligi kati ya Yanga na Azam FC umepangwa kupigwa saa 10 jioni, na unatarajiwa kuwa mmoja kati ya mechi zenye ushindani mkali zaidi katika msimu huu wa Ligi Kuu.



