Yanga SC waliendelea kuthibitisha ubora wao kwenye ligi kuu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo uliopigwa mkoani Kigoma, matokeo ambayo yamewapa nafasi nzuri zaidi kileleni mwa msimamo wa NBC Premier League.
Bao la kwanza la Yanga SC lilipatikana dakika ya 28 kupitia kiungo Mudathir Yahya, aliyefunga kwa shuti kali nje ya eneo la hatari baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Prince Dube.
Kipindi cha kwanza kilishuhudia Yanga wakitengeneza nafasi zaidi, lakini Maxi Nzengeli na Dube walikosa kutumia nafasi muhimu zilizoweza kuipa timu yao uongozi mkubwa mapema.
Kipindi cha pili, Yanga walionekana kupunguza kasi na kuwapa nafasi Mashujaa FC kutawala sehemu ya mchezo, hali iliyofanya mchezo kuwa na ushindani zaidi huku wenyeji wakijaribu kusaka bao la kusawazisha. Hata hivyo, ulinzi wa Yanga uliendelea kuwa imara na kuzuia mashambulizi mengi ya wapinzani wao.
Mchezo ulipofika dakika za mwisho, Yanga waliongeza bao la pili kupitia nahodha wao Bakari Mwamnyeto, aliyemaliza kwa ustadi baada walinzi wa Mashujaa Fc kushindwa kushindwa kuondoa hatari langoni.
Ushindi huo unaifanya Yanga SC kujiimarisha kileleni mwa ligi wakiwa na tofauti ya pointi tano dhidi ya wapinzani wao wa jadi Simba SC bada ya kufikisha alama 63.
Simba wanatarajiwa kucheza dhidi ya Pamba Jiji FC katika mchezo utakaopigwa siku ya Jumapili.
Katika mchezo mwingine wa mapema, Mbeya City FC waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar FC, matokeo ambayo yanaendelea kuwapa matumaini ya kupambana kuhakikisha wanabaki katika ligi kuu msimu ujao.



