Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Akizungumza kuelekea pambano hilo, Barker amesema maandalizi ya timu yamekamilika na wachezaji wako katika hali nzuri ya kupambana kutafuta ushindi ambao ni muhimu katika mbio za ubingwa wa ligi msimu huu.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza kati ya mechi tano zilizosalia kwa Simba, huku Wekundu wa Msimbazi wakihitaji kushinda michezo yote ili kuendelea kuweka presha kwa watani wao wa jadi Yanga kwenye kinyang'anyiro cha ubingwa.
"Sisi tuko tayari, tumepata muda mzuri wa kujipanga vyema kwa mechi hii na mechi zote zilizosalia hadi mwisho wa msimu," alisema Barker.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisisitiza kuwa lengo kuu la Simba ni kupata alama tatu licha ya kutambua kuwa watakutana na upinzani mkubwa kutoka kwa Pamba Jiji.
"Malengo yetu ni kupata alama tatu kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Pamba Jiji. Tunajua hautakuwa mchezo mwepesi," aliongeza.
"Tunajua tutakutana na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wetu, lakini tuko tayari kupambana na kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo huo."
Mashabiki wa Simba watakuwa na matumaini makubwa kuona timu yao ikiendeleza kasi ya ushindi na kuendelea kufukuzia ndoto ya kutwaa ubingwa hadi dakika za mwisho za msimu.



