Kaseja airejesha Kagera Sugar Ligi Kuu, Geita Gold nayo yarudi rasmi

Joel JJ By Joel JJ β€’ 8th June 2026


Kaseja airejesha Kagera Sugar Ligi Kuu, Geita Gold nayo yarudi rasmi

Kocha Juma Kaseja ameiongoza Kagera Sugar kurejea rasmi Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao baada ya timu hiyo kupata ushindi muhimu wa mabao 3-0 dhidi ya KenGold katika mchezo wa raundi ya 28 wa Championship.

Matokeo hayo yamehitimisha safari ya kusisimua ya Kagera Sugar katika msimu huu, huku timu hiyo ikifikisha pointi 68 na kujihakikishia nafasi ya kupanda daraja moja kwa moja kabla ya kumalizika kwa ligi.

Mafanikio ya Kagera Sugar yamekuja sambamba na matokeo yasiyokuwa mazuri kwa wapinzani wao wa karibu, Polisi Tanzania, ambao walipoteza mchezo wao dhidi ya Mbuni FC. Matokeo hayo yameifanya Polisi kubaki na nafasi ya kufikisha pointi 66 pekee katika mechi mbili zilizobaki, idadi ambayo haiwezi tena kuifikia Kagera Sugar.

Ni mafanikio makubwa kwa Kaseja ambaye katika msimu wake wa kwanza akiwa kocha mkuu ameonyesha uwezo mkubwa wa kuijenga timu yenye ushindani. Tangu kuanza kwa msimu huu, Kagera Sugar imekuwa miongoni mwa timu zilizotawala Championship kwa kucheza soka la uhakika na matokeo ya kuvutia.

Katika mechi 28 walizocheza hadi sasa, Kagera Sugar imeandika ushindi 21, sare tano na kupoteza michezo miwili pekee, rekodi inayoonyesha uimara wao katika mbio za kurejea ligi kuu.

Wakati Kagera Sugar ikisherehekea kurejea kwenye ligi ya juu, Geita Gold FC nayo imefanikiwa kutimiza lengo lake la kupanda daraja baada ya kuifunga Songea United mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

Ushindi huo umeifanya Geita Gold kufikisha pointi 71 na kujihakikishia nafasi katika mbili bora za Championship, nafasi zinazotoa tiketi ya moja kwa moja ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2026/27.

Timu hiyo imeonyesha uthabiti mkubwa tangu mwanzo wa msimu na imekuwa miongoni mwa vinara wa msimamo kwa muda mrefu, jambo lililowezesha kufanikisha azma ya kurejea haraka kwenye ligi kuu.

Kurejea kwa Geita Gold na Kagera Sugar kunatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika Ligi Kuu msimu ujao, huku timu zote mbili zikitarajiwa kutumia uzoefu walioupata Championship kujenga vikosi vitakavyoweza kuhimili ushindani wa ngazi ya juu.

Kwa Kagera Sugar, mafanikio haya yanaipa sifa kubwa benchi la ufundi linaloongozwa na Juma Kaseja, ambaye ameonyesha uwezo wa kuibadilisha timu hiyo ndani ya muda mfupi na kuirejesha mahali inapostahili kuwa.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.