Ibenge ajiondoa mchakato wa uteuzi wa kocha Mali

Joel JJ By Joel JJ • 2nd June 2026


Ibenge ajiondoa mchakato wa uteuzi wa kocha Mali

Kocha Mkuu wa Azam Fc, Jean-Florent Ibenge, hatakuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Mali baada ya kujiondoa katika mchakato wa uteuzi akiwa hatua za mwisho kabisa.

Taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Mali, Fédération Malienne de Football (FEMAFOOT), zimeeleza kuwa Ibenge alikuwa ameshafikia hatua ya juu katika mazungumzo na hata kuchaguliwa kama mgombea namba moja kwa ajili ya kuchukua mikoba ya timu ya taifa, maarufu kama “The Eagles”.

Hata hivyo, ghafla kocha huyo ameamua kujiondoa kwenye mchakato huo akitaja sababu za kifamilia zilizopelekea kushindwa kuendelea na majukumu hayo mapya. Uamuzi huo umeibua mshangao mkubwa ndani ya uongozi wa soka nchini Mali, hasa kwa kuwa mchakato ulikuwa umefikia hatua ya mwisho kabisa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi wa FEMAFOOT wamesikitishwa na hatua hiyo wakiamini kuwa muda muhimu umepotea katika kipindi ambacho walitarajia kumtangaza kocha mpya. Baadhi ya maafisa wanahisi kwamba kama changamoto za kifamilia zilikuwepo, Ibenge alipaswa kuzibainisha mapema kabla ya kufikia hatua ya makubaliano ya juu.

Inaelezwa kuwa Ibenge alipitia hatua zote za usaili na tathmini, na alikuwa amepitishwa kama chaguo bora la kuinoa Mali, lakini alitoa taarifa ya kujiondoa wakati mazungumzo yakiwa yamekaribia kukamilika.

Kwa sasa, Shirikisho la Soka la Mali linaendelea tena na mchakato wa kutafuta kocha mpya, huku likilazimika kurejea orodha ya wagombea wengine waliokuwa wamepita awali. 

Inaelezwa Azam Fc imepiga hatua kubwa kumshawishi Ibenge na huenda akaongeza mkataba kuendelea kuinoa Azam Fc.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.